Jumapili 4 Oktoba 2026 - 17:10
Mufti wa Uganda Azindua Wilaya ya Kiislamu ya Zombo

Hawza/ Mufti wa Uganda, Dkt. Sheikh Shaban Ramadhan Mubaje, amezindua rasmi Wilaya mpya ya Kiislamu ya Zombo katika eneo la West Nile, hatua inayowapa Waislamu wa eneo hilo muundo wao huru wa kiutawala.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, uzinduzi huo ulifanyika siku ya Ijumaa, tarehe 2 Oktoba 2026 (10 Mehr 1404 H.S), katika Halmashauri ya Mji wa Warr, Wilaya ya Zombo, karibu na mpaka wa Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Katika uzinduzi huo Mufti wa Uganda, aliandamana na Naibu Mufti wa Pili, Mheshimiwa Dkt. Sheikh Hafiz Muhammad Harunah Bukenya; Naibu Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu la Uganda (UMSC) anayesimamia Fedha na Utawala, Wakili Haj Muhammad Ali Aluma; Katibu wa Masuala ya Dini, Sheikh Imran Ssali; pamoja na Sheikh Abdul-Karim Abdallah Katamba, Mkuu wa Idara ya Halal ya Baraza la Waislamu la Uganda (UMSC) na Msaidizi wa Kikanda wa Mufti kwa Ankole-Kigezi.

Ujumbe huo ulipokelewa Alhamisi jioni na umati mkubwa wa Waislamu pamoja na watu wa dini nyingine, katika ziara ya kwanza ya Mufti mjini Warr. Miongoni mwa walioupokea ujumbe huo walikuwa Sheikh Mahdie Mahmood Raihan, Msaidizi wa Kikanda wa Mufti kwa West Nile; Sheikh Abdul-Azziz Qaasim Al Kuriy, Kadhi mwenyeji; Jenerali Dick Olum, afisa mwandamizi wa jeshi; pamoja na viongozi wengine wa serikali.

Siku hiyo ya Ijumaa, mamia ya Waislamu, wakiwemo wanafunzi wa shule, waliungana na Mufti pamoja na ujumbe wake kutembelea taasisi za Baraza la Waislamu la Uganda (UMSC) zilizopo eneo hilo. Taasisi hizo ni pamoja na Kituo cha Afya cha Kiislamu cha Warr cha Daraja la Pili, Shule ya Msingi ya Kiislamu ya Warr, na Shule ya Awali na Msingi ya Kiislamu ya Daru Habib. Ujumbe huo pia ulitembelea jengo la kihistoria ambalo hapo zamani lilikuwa makazi na duka la Sheikh Sharif Said, mwanazuoni wa Kiislamu aliyekuwa anatokea Mombasa, Kenya.

Mufti wa Uganda Azindua Wilaya ya Kiislamu ya Zombo

Sheikh Sharif Said anakumbukwa kuwa miongoni mwa Waislamu wa kwanza kuishi katika eneo hilo, na alitekeleza wajibu mkubwa katika kueneza Uislamu, ambao tangu wakati huo umekua na kuwa na jamii kubwa. Baadaye, Mufti alijiunga na mamia ya Waislamu na wageni wengine waliokusanyika kwa ajili ya sherehe za uzinduzi chini ya mahema yaliyowekwa katika uwanja wa Msikiti Mkuu.

Wakili Hadad Salim, Kamishna Huru wa Uchaguzi wa Baraza la Waislamu la Uganda, kwa Kanda ya West Nile, alitangaza rasmi kuzinduliwa Wilaya ya Kiislamu ya Zombo pamoja na uteuzi wa Kadhi wake wa kwanza. Alisema kuwa mabadiliko hayo ya kiutawala yalifanywa kwa mujibu wa Katiba ya Baraza la Waislamu la Uganda. Katika hotuba yake ya uzinduzi, Sheikh Abdul-Azziz alimshukuru Mufti kwa kuipatia Zombo hadhi ya Wilaya ya Kiislamu, huku akibainisha kuwa hapo awali eneo hilo lilikuwa chini ya utawala wa Nebbi.

“Tumepewa utambulisho wa kiutawala ambao tulikuwa tukiusubiri kwa muda mrefu. Kwa hiyo, sasa tunapaswa kujenga taasisi inayostahili utambulisho huo,” alisema Sheikh Abdul-Azziz, huku akitoa wito wa kuungwa mkono ili kuimarisha wilaya hiyo mpya.

Viongozi kadhaa wa serikali na jamii walihudhuria hafla hiyo, wakiwemo Wabunge Grace Freedom Kwiyucwiny, Topista Acamfua na Gabriel Okumu; Oyulu Oruna James; Kamishna Mkazi wa Wilaya, Ayikobuwa Festos; Jenerali Dick Olum; pamoja na mwakilishi wa Ufalme wa Alur. Viongozi hao waliahidi kushirikiana kwa karibu na uongozi wa Wilaya mpya ya Kiislamu ya Zombo.

Sheikh Mahdie Mahmood Raihan aliwapa washiriki taarifa kuhusu hali ya Waislamu katika Kanda ya West Nile, huku Wakili Aluma akitoa taarifa ya maendeleo katika makao makuu ya Baraza la Waislamu la Uganda.
Mufti, akihutubia mkutano huo kwa Kiswahili, aliwashukuru Waislamu na wakazi wengine wa Zombo kwa mapokezi yao ya ukarimu. Pia alieleza changamoto ambazo Baraza la Waislamu la Uganda, ilikabiliana nazo kabla ya yeye kuingia madarakani, pamoja na juhudi zilizofanywa kuimarisha na kurejesha hadhi ya taasisi hiyo.

Aidha, Mufti aliishukuru serikali, viongozi wa eneo hilo na jamii pana ya Zombo kwa kuunga mkono ushirikiano baina ya waumini wa dini tofauti na kufanya kazi pamoja katika kuendeleza kuishi kwa amani.

Mufti huyo pia alijibu kwa mtazamo chanya maombi kadhaa yaliyotolewa na viongozi wa eneo hilo, ikiwemo hitaji la dharura la kujengwa shule ya sekondari ya Kiislamu katika eneo hilo.
Vilevile, aliahidi kuunga mkono juhudi za kuziwezesha wilaya nyingine mpya za Kiislamu katika West Nile kuanza kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
Kabla ya kuondoka Zombo, Mufti na ujumbe wake walikaribishwa kwenye chakula cha mchana na Jenerali Olum katika hoteli yake mpya ya nyota tatu. Kama ishara ya heshima na urafiki, Jenerali Olum aliipa moja ya sehemu za hoteli hiyo pamoja na nyumba moja ya malazi jina la Mufti. Sehemu hizo zimekusudiwa kuwahudumia wageni Waislamu kwa kuzingatia maadili na kanuni za Kiislamu.

Baadaye, Mufti na ujumbe wake waliondoka Zombo kuelekea Jiji la Lira, kaskazini mwa Uganda.

Chanzo: Baraza Kuu la Waislamu la Uganda (UMSC).

Mufti wa Uganda Azindua Wilaya ya Kiislamu ya Zombo

Mufti wa Uganda Azindua Wilaya ya Kiislamu ya Zombo

Mufti wa Uganda Azindua Wilaya ya Kiislamu ya Zombo

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha